WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, amewataka watendaji wa Wizara, Idara na Taasisi zilizomo katika wizara hiyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuongeza ufanisi.
Rai hiyo ameitoa huko katika Kikao na watendaji hao kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo Maruhubi, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Shamata alisema lengo la kikao hicho ni kuwakumbusha watendaji hao watambue majukum yao katika kazi zao pamoja na kuhakikisha wanaongeza ufanisi mkubwa katika shughuli zao za kazi
Aliongeza kuwa serikali ina dhamira ya kuhakikisha kuwa Zanzibar inaongeza uzalishaji wa mazao muhimu ili kupunguza utegemezi na uagizaji wa bidhaa za chakula na mazao yanayotokana na Kilimo kutoka nje.
Aidha aligusia kwa upande wa tafiti zinazofanyika na kuwataka wataalam kuhakikisha matokeo yake yanawafikia wakulima ambao wanategemea kutumia tafiti hizo kulima kisasa na kuongeza tija kwenye kilimo chao.
“Lazima tuwe na mkakati wa utafiti kwani hatuwezi kuzalisha kwa ufanisi pasi na kua na tafiti, hivyo kila taasisi za utafiti zishirikiane kujua kilichofanikiwa ili tuweze kuona tija iliyopatikana”, alisema Shamata
Sambamba na hayo Shamata aliwataka watendaji hao kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima na kuzalisha kwa wingi mazao mbali mbali kujipatia lishe na kipato.
Nae Afisa Mkuu wa Utumishi wa wizara hiyo, Masoud Salum Abdi, akizungumza kwa niaba ya watendaji wenziwe, alimshukuru Waziri Shamata kwa kuitisha kikao hicho katika kuendeleza mashirikiano pamoja na miongozo aliyoitoa ya kuweza kuboresha maagizo ya kutekeleza majukum yao
Aidha alihidi kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa yakiwemo ya kupunguza utegemezi wa kuagiza vyakula kabla ya kufika mwaka 2025 kuwe na matokeo ya mfano kama ilivyoelezwa katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025.