Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar ZARI kwa kushirikiana na Taasisi ya kimataifa ya Mazao ya Joto imefanya Tafiti za Tathmini mbegu bora za muhogo ili kukabiliana na athari za maradhi ya michirizi ya kahawia ya muhogo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar Dkt. Mohamed Dhamir Kombo ameeleza hayo huko Kizimbani Wilaya ya Magharibi A Unguja alipokua akizungumza na watafiti, mabwana shamba na wakulima wakati wa uvunaji wa zao la muhogo uliopatikana katika utafiti huo.
Amesema hatua hiyo imehusisha tathmini ya mbegu za muhogo zinazostahamili maradhi ambapo taasisi hizo zimefanya Jumla ya tafiti za aina 8 za mbegu hizo zilizofanywa kwa mwaka mzima kwa ajili ya kuzifanyia majaribio ya ustahamilivu wa maradhi ya michirizi ya kahawia ambayo imekua ni changamoto kubwa inayowakabili wazalishaji wa zao hilo na kusababisha uhaba wa mavuno na hivyo kuathiri kipato cha wakulima. Amesema muhogo unapokuwa na tatizo la maradhi hayo uzalishaji hupungua kwa kiasi kikubwa hivyo ni vyema wataalamu wa kilimo pamoja na wakulima wawe ni kiungo katika uzalishaji sambamba na kutatua changamoto ya magojwa katika zao hilo.
“Mategemeo yangu mtakua na mashirikiano katika utunzaji wa mbegu hizi kwa vile uwepo wenu utaweza kusaidia katika kuona aina za mbegu zilizo na tatizo na zisizo na tatzo kwani nyinyi mna ujuzi wa taaluma ya asili inayohusiana na udhibiti wa matatizo ya magojwa katika muhogo, amesema Mkurugenzi huyo” Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Taasisi hiyo Salma Omar Mohd amewashauri wakulima hao wafanye uchaguzi sahihi wa mbegu hizo ili kupata mbegu bora zenye uzazi mkubwa na ambazo zinazostahamili maradhi na ukame Aidha Salma amewataka wakulima hao kua mabolozi kwa wenzao waliokua hawajafika katika tukio hilo kwani matarajio yao kuwa mbegu hizo walizopatiwa wajitahidi kuzizalisha kwa wingi ili waweze kuwapatia wakulima wengine kwa Upande wa Unguja na Pemba.
Nae bwana shamba wa mkoa wa kaskazini Unguja Ame Khamis Ame ameeleza kuwa zoezi la uvunaji wa mbegu hizo ni muhimu ambapo limefanywa kwa wakati muafaka kwani wakulima wengi wamekosa uzalishaji kutokana na mbegu nyingi zilizomo mashambani zimeathirika na maradhi ya michirizi ya kahawia hivyo kutolewa kwa aina 8 mpya za mbegu hizo zitaweza kuwaokoa wakulima na kuweza kuzalisha muhogo kwa wingi .
Mapema akizungumza mkulima kutoka machui Ameir Salum Juma kwa niaba ya wakulima wenziwe ametoa shukran kwa Taasisi hiyo kwa kuwapatia mbegu hizo kwani zitaenda kuwasaidia katika kuwazalishia mbegu mpya ambayo matarajio yao baada ya kupata mbegu hizo uzalishaji wa muhogo utaanza upya na kwa kasi zaid na utaweza kuwaletea mafanikio makubwa ya kuwapatia kipato chao na taifa kwa ujumla.